Shirika la AGPAHI lafanya mkutano na wabunge wanaotoka mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Geita, mjini Dodoma

Shirika la Kitanzania lisilo la kiserikali la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative( AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI limefanya mkutano na wabunge wanaotoka mikoa ya Shinyanga , Simiyu na Geita kwa lengo la kuwafahamisha watunga sera kazi zinazofanywa shirika hilo katika mikoa hiyo ikiwa ni pamoja na kuainisha mafaniko yaliofikiwa katika kipindi cha miaka mitano (5)tangu lilipoanza kutekeleza miradi yake mwaka 2011. 

Mkutano huo umefanyika siku ya Jumanne, Agosti 23, 2016 mjini Dodoma ukiwa ni wa tatu kufanyika tangu kuanzishwa kwa shirika la AGPAHI mwaka 2011, likifadhiliwa na watu wa Marekani kupitia mashirika ya Centres for Disease Control and Preventation (CDC); shirika la misaada la Marekani (USAID); Mfuko wa kusaidia watoto wenye VVU kwa hisani ya watu wa Uingereza (CIFF) na Mfuko wa Idadi ya watu duniani (UNFPA).

Miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ni wawakilishi wa kamati ya Bunge inayoshuhulika na masuala ya Ukimwi (TAPAC) na wabunge waliohudhuria mkutano huo ni Mhe. Stanslaus Nyongo, Mhe. Esther Midimu, Mhe. Ezekiel Maige, Mhe. Augustino Masele, Mhe. Elias Kwandikwa, Mhe. Dunstan Kitandula na Mhe. Shally Raymond.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGPAHI, Dr. Sekela Mwakyusa aliwaeleza waheshimiwa wabunge kuwa miongoni mwa kazi zinazofanywa na AGPAHI kuwa ni pamoja na kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) hususani kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kutoa huduma ya matunzo na tiba kwa watu wanaoishi na VVU katika mikoa ya Shinyanga , Simiyu na Geita.

Dr. Mwakyusa aliongeza kuwa kwa kufuata mwongozo wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na watoto pia wanatoa huduma ya uchunguzi na huduma ya awali ya tiba ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa huduma za afya ya uzazi na uzazi wa mpango.

Alibainisha kuwa AGPAHI imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya 14 katika mikoa husika pamoja na vituo vya afya,zahanati,hospitali za taasisi za kidini,binafsi na za serikali.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwezi Oktoba mwaka 2015 hadi Juni 2016, shirika limefanikiwa kuwapima VVU akina mama wajawazito 128,806 ambapo kati yao akina mama 3,709 walikutwa na maambukizi ya VVU na kuanzishiwa huduma ya dawa.

"Katika kipindi hicho hicho,pia shirika limeweza kuwafikia watoto wapatao 3,182 na kuwaanzishia huduma ya tiba na tumeweza kujenga na kuboresha majengo ya kutolea huduma ya matunzo na tiba (CTC) katika vituo mbalimbali kama vile vituo vya Kambarage, Maganzo, Nindo, Kagongwa, Mbogwe, Mipa, Somagedi na Segese",alieleza Dr. Mwakyusa.

"Kwa kutambua umuhimu wa vitendea kazi, shirika limekabidhi magari matano mapya katika halimashauri za wilaya za Meatu, Busega, Itilima, Kishapu na Msalala ambayo hutumika katika halmashauri za wilaya husika kuboresha utendaji kazi wa miradi ya Ukimwi na kuwafikia watu wengi katika huduma",aliongeza.

Alisema shirika pia limetoa pikipiki 8 na baiskeli 104 kwa watoa huduma za afya ili kusaidia kuboresha huduma katika ngazi ya vituo, jamii na familia kwa kusafirisha sampuli kutoka kituo kidogo hadi kikubwa na kutafuta wateja waliopotea kwenye huduma.

Aliongeza kuwa mbali na kutoa vitendea kazi, shirika hilo limekuwa likitoa mafunzo kwa watoa huduma za afya na wafanyakazi wa halmashauri ambako miradi yao inatekelezwa sambamba na kufanya uhamasishaji wa upimaji wa virusi vya ukimwi kwa njia ya kampeni kwa lengo la kuwafikia watu wengi zaidi hususani waliopo maeneo ya vijijini.

Dr. Mwakyusa alitumia fursa hiyo kuwafahamisha wabunge kuwa mradi wa sasa ambao ulikuwa ni wa miaka mitano unafikia ukomo mwezi Septemba mwaka huu.


Hata hivyo alisema shirika limepata mradi mwingine ambapo mikoa ya utendaji kazi itaongezeka kutoka mikoa mitatu na kuwa sita ambayo ni Shinyanga, Simiyu, Geita, Mara, Mwanza na Tanga.

Nao wabunge waliohudhuria mkutano huo walilishukuru shirika la AGPAHI kwa huduma nzuri ambazo limekuwa likitoa kwa wananchi katika kuhakikisha kuwa maambukizi ya VVU yanapungua na hata kuisha kabisa katika jamii.

“Ushirikiano uliopo ni mzuri ,tunaomba shirika hili liendelee kushirikiana na viongozi mbalimbali kama mlivyofanya kwa sisi wabunge ili kusaidia na kuwafikia wananchi wengi zaidi" ,alisema Mhe. Augustino Masele (Mbunge wa Mbogwe mkoani Geita).

Masele alieleza kuwa wilaya ya Mbogwe ina wachimbaji wadogo wadogo wengi hivyo itakuwa vyema kama shirika hilo litawapa kipaumbele kwenye mradi ujao.

“Familia nyingi zimekuwa zikiwaachia watoto wasio na elimu ya kuhudumia wagonjwa hivyo kujikuta wanapata maambukizi , elimu zaidi inahitajika kwenye jamii haswa kwenye familia zenye wagonjwa, watambue namna sahihi ya kutoa huduma kwa mgonjwa na kuto waachia watoto”, aliongeza Mhe. Esther Midimu (mbunge viti maalum Simiyu).

Mheshimiwa Midimu alishauri kampeni za upimaji zifanyike kwa wanafunzi walioko vyuoni ili watambue hali za afya zao huku akiomba kushirikishwa kwenye kampeni mbalimbali za utoaji elimu ya Ukimwi.

Naye Mhe. Stanslaus Nyongo alishukuru kwa kushiriki katika mkutano huo kwani umempa taarifa nyingi kuhusu miradi ya AGPAHI wilayani Maswa mkoani Simiyu na kuahidi kufuatilia kazi za miradi ya AGPAHI kwa ukaribu na kuomba kushirikishwa kwenye programu mbalimbali za utoaji elimu kwenye jimbo lake la Maswa Mashariki.


Kwa upande wake Mbunge wa Msalala,mkoani Shinyanga Mhe. Ezekiel Maige ambaye tayari wananchi wake wananufaika na miradi ya shirika hilo,alisisitiza shirika hilo liendelee kujitangaza kwani kazi inayofanyika kwenye mikoa husika ni nzuri kwani inagusa maisha ya watanzania moja kwa moja.


Mhe. Maige aliliomba shirika hilo kuendelea kutoa msisitizo wa upimaji VVU wa pamoja wa baba na mama (couple testing) kwani inasaidia sana kujua afya zao na ni yvema faida za upimaji wa pamoja zikaainishwa ili wananchi waelewe faida za upimaji wa pamoja.

“Nawakaribisheni sana Tanga, na ninaahidi kufanya kazi nanyi kwa ukaribu zaidi,nimefurahi sana na nitajitahidi kuhakikisha mnashiriki kwenye kikao cha ushauri wa mkoa (RCC) Tanga pamoja na vikao vya baraza la madiwani Tanga",alieleza Mhe. Dunstan Kitandula (mwenyekiti wa TAPAC ambaye ni mbunge wa Mkinga). 

“Napongeza sana kwa juhudi zenu kwenye mikoa husika, tatizo bado ni kubwa, akina mama wanaendelea kunyanyasika , kwani akina baba ni wagumu sana kwenda kupima na pindi mwanamke anapobainika kuwa ana VVU hupigwa na kufukuzwa , bado elimu inahitajika kwa kina baba kuelewa umuhimu wa wote kupima na kukubaliana”, Mhe. Shally Raymond (TAPAC).

Angalia picha hapa chini yaliyojiri katika mkutano huo uliofanyika mjini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGPAHI, Dr. Sekela Mwakyusa akielezea kazi za shirika kwenye kikao na wabunge kutoka mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Geita.

Wabunge wanaotoka mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Geita wakiwa ukumbini.

Mhe. Elias Kwandikwa (Mbunge jimbo la Ushetu) akisoma moja ya ripoti ya Shirika za AGPAHI 

 

Kutoka kulia ni Mhe. Stanslaus Nyongo, Mhe. Esther Midimu na Mhe. Shally Raymond

 


Mhe. Mhe. Stanslaus Nyongo akisisitiza jambo.

Mhe. Dunstan Kitandula (Mbunge) akielezea jambo ukumbini

 

Mhe. Ezekiel Maige (Mbunge jimbo la Msalala) akizungumza katika mkutano huo

 

Mhe. Dunstan Kitandula (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGPAHI, Dr. Sekela Mwakyusa

 

Picha ya pamoja ya wabunge waliohudhuria mkutano huo wakiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Dr. Sekela Mwakyusa mjini Dodoma

 

Source: http://www.malunde.com

 

More on News

Get Connected