KAMBI YA WATOTO KUTOKA GEITA,MWANZA NA SHNYANGA YAFUNGWA RASMI

Kambi ya Watoto na Vijana “Ariel Camp” iliyoandaliwa na shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi iliyoanza June 19,2017 jijini Mwanza imefungwa leo Ijumaa June 23,2017.

Kambi hiyo ilikutanisha watoto na vijana 50,walezi 11 walioambana nao kutoka mikoa ya Shinyanga,Mwanza na Geita. Miongoni mwa mambo waliyojifunza katika kambi hiyo iliyodumu kwa muda wa siku tano ni pamoja na lishe,ufuasi mzuri wa dawa,unyanyapaa na ubaguzi,haki na wajibu wa watoto pamoja na elimu ya afya ya ujana na makuzi. Washiriki wa kambi hiyo pia walitembelea makumbusho ya Wasukuma ya Bujora na kufanya michezo mbalimbali nje ya darasa yenye kuashiria umoja,ushirikiano,upendo na kujenga mtazamo chanya kwenye maisha yao.

Akizungumza wakati wa kufunga kambi ya nane ya Ariel jijini Mwanza,mgeni rasmi,Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Dk. Silas Wambura, aliwataka watoto na vijana hao kuwa mabalozi wazuri wanaporudi nyumbani huku akiwasihi kuzingatia masomo na kanuni za afya ili kufikia malengo yao ya kimaisha.

Katika hatua nyingine,Dk. Wambura alisema serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na shirika la AGPAHI katika sekta ya afya na kwamba serikali itaendelea kushirikiana nao ili watanzania wengi zaidi waweze kunufaika na huduma zinazotolewa na shirika hususani katika mapambano ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi.

 

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi kutoka AGPAHI,Dk. Safila Telatela alisema takribani watoto na vijana 400 wameshapata fursa ya kushiriki Kambi ya Ariel ambao hutoka kwenye klabu za vijana na watoto kwenye mikoa wanayotoka. “Hii ni kambi ya nane tangu kuanza kwa shirika letu mwaka 2011,tulianza kufanya kazi katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu,na kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2016,tuliongeza mikoa minne ya Mwanza,Tanga,Geita na Mara hivyo kufikisha idadi ya mikoa sita ambako tunafanya kazi”.

“Mshiriki wa kambi lazima awe mwanachama wa klabu za vijana na watoto,lakini kwa mikoa hii mipya (Mwanza,Geita,Tanga na Mara),shirika liliamua kuwachukua vijana,watoto na walezi kushiriki kwenye kambi ndipo baadae kuanza mchakato wa kuunda klabu/vikundi ili kutoa huduma za kisaikolojia kwa watoto”,aliongeza Dk. Telatela.

   Katika hatua nyingine alisema AGPAHI linatekeleza majukumu yake kwa hisani ya Watu wa Marekani kupitia shirika la Centres for Disease Control and Preventation (CDC),mfuko wa kusaidia Watoto wenye VVU Kwa hisani ya watu wa Uingereza (CIFF) na Shirika la Development Aid From People to People (ADPP - Mozambique).

 

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA KUFUNGA KAMBI YA ARIEL MWAKA 2017 JIJINI MWANZA

 Mgeni rasmi,Dk. Silas Wambura,Mkurugenzi wa Miradi AGPAHI, Dk. Safila Telatela na watoto walioshiriki Kambi ya Ariel wakikata keki.

Mtoto akielezea jinsi alivyofurahishwa na mambo mbalimbali akiwa kambini.

 

 

 Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Mwanza,Dk. Silas Wambura akiangalia michoro ya miti ya maisha iliyochorwa na watoto na vijana walioshiriki kambi ya Ariel wakielezea kwa ufupi mambo wanayoyapenda katika maisha yao.

Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Geita,Richard Kambarangwe akimwelezea mgeni rasmi,Dk. Wambura kuhusu shindano la 'Mkali Wao' ambapo washiriki hushindanishwa katika masuala mbalimbali mfano kujiamini,ucheshi,usikivu, utulivu,uchezaji mzuri wa muziki,kujibu maswali vizuri,uongozi mzuri,kutunza muda,nidhamu na utii na uchangamfu kambini na mshindi anayepatikana hupigwa picha katika bango hilo.

   Picha ya pamoja: Mgeni rasmi na watumishi wa afya waliombatana na watoto na vijana kutoka mikoa ya Shinyanga,Mwanza na Geita

 

Picha ya pamoja: Mgeni rasmi na wafanyakazi wa AGPAHI. 

 Vijana wakicheza muziki

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

More on News

Get Connected