MALUMBANO YA HOJA KWA VIJANA YAENDESHWA NA AGPAHI MKOANI SHINYANGA

Ijumaa Julai 28,2017 Vijana wamekutana katika Ukumbi wa Karena Hotel mjini Shinyanga kwa ajili ya Malumbano ya Hoja kuhusu Vijana kujadili kuhusu utaratibu wa kupambana na kudhibiti maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU),unyanyapaa na vifo vinavyotokana na UKIMWI nchini Tanzania.

Mratibu wa Masuala ya Watoto AGPAHI mkoa wa Shinyanga,Dk. Jane Kashumba akizungumza wakati wa Malumbano ya Hoja kwa vijana yaliyoandaliwa na shirika hilo katika ukumbi wa Karena Hotel mjini Shinyanga

Malumbano hayo ya Hoja yaliyoandaliwa na shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi kupitia kwa ufadhili wa mfuko wa kusaidia Watoto wenye VVU Kwa hisani ya watu wa Uingereza (CIFF) yamekutanisha vijana kutoka wilaya ya Kahama,Kishapu na Shinyanga.

Wakichangia hoja,vijana hao mbali na kulipongeza shirika la AGPAHI na serikali katika kuboresha huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma pia waliishukuru AGPAHI kwa kusaidia watu wanaoishi na maambukizi ya VVU. Vijana hao walisema ili kuhakikisha mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi yanafanikiwa ni vyema suala la elimu kuhusu Ukimwi likatiliwa mkazo katika maeneo yote mjini na vijijini kwani vifo vingi vinatokea kutokana na jamii kutokuwa na elimu sahihi.

Elimu sahihi kuhusu Ukimwi bado haijatolewa kwa pande zote mbili za watu wanaoishi na maambukizi ya VVU na wale wasio na maambukizi ya VVU,elimu ikitolewa watu hawatapata maambukizi mapya,watu watazingatia matumizi sahihi ya dawa na hapatakuwa na unyanyapaa”,walieleza vijana hao.

Watu hawajitokezi kupima afya zao hali ambayo inachangia kuwepo kwa vifo vinavyotokana na Ukimwi,watu hao wangepata elimu sahihi wangeweza kuanza kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU lakini kutokana na kutojua afya zao wengine wanakuwa na imani za kishirikina kwamba wamerogwa kumbe wamejiroga wao wenyewe kwa kutopima afya zao”,waliongeza vijana hao.

Katika hatua nyingine vijana hao waliitaka serikali kuboresha mazingira katika shule kwa kuwajengea mabweni wanafunzi wa kike ili kuwaepusha na vishawishi wanaposafiri umbali mrefu kutoka majumbani kwao kwenda shuleni. “Tunaomba wanafunzi wajengewe mabweni kwani wapo wanafunzi wanaopata vishawishi wakiwa njiani lakini wengine kutokana na hali ngumu ya maisha wanajikuta wanaingia katika mahusiano ya kimapenzi matokeo yake wanapata maambukizi ya VVU”,walisema.

Naye Mratibu wa Masuala ya Watoto AGPAHI mkoa wa Shinyanga,Dk. Jane Kashumba alisema lengo la Malumbano hayo ya Hoja ni kutaka kujua vijana wanahitaji nini ili kuhakikisha mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi yanafanikiwa nchini Tanzania. “Sisi tunajihusisha na mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,tunatamani kuona watoto wote walio na maambukizi wanapata huduma za afya lakini pia kuhakikisha vijana wanatumia dawa na wale vijana waliopo katika jamii wanapima afya zao”,alieleza Dk. Kashumba.

“Tunatambua uwepo wa vijana ndiyo maana tumeona ni vyema tuwe na Malumbano ya hoja na vijana ili tuweze kujua wanaelewa kiasi gani kuhusu huduma rafiki zinazopatikana katika vituo vyetu vya kutolea huduma na pia tuone je wanaonaje utaratibu wa kupambana na kudhibiti maambukizi mapya ya VVU,unyanyapaa na vifo dhidi ya Ukimwi kama unafanyika ipasavyo nchini”,aliongeza Dk. Kashumba.

Akizungumza wakati wa Malumbano hayo ya Hoja,Mgeni Kaimu Mratibu wa Ukimwi mkoa wa Shinyanga Sherida Madanka alisema malumbano hayo ni fursa nzuri kwa vijana kujieleza na kutoa maoni yao nini kifanyike katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi katika jamii. “Nawapongeza sana vijana kwa uwezo mlionao wa kujieleza katika masuala ya VVU na Ukimwi naamini kupitia elimu hii ya kutosha mliyonayo mtaitumia kuielimisha jamii ili kuhakikisha kuwa maambukizi mapya yanapungua”,alieleza Madanka.

Katika hatua nyingine Madanka aliwasihi watu wanaoishi na VVU kujiamini sambamba na kuwa wafuasi wazuri wa dawa ili kufikia malengo yao huku akiwasisitiza wananchi kujitokeza kupima afya zao.

Shirika la AGPAHI linatekeleza shughuli zake katika mikoa ya Shinyanga,Simiyu,Mwanza,Tanga,Geita na Mara kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia shirika la Centres for Disease Control and Preventation (CDC),mfuko wa kusaidia Watoto wenye VVU Kwa hisani ya watu wa Uingereza (CIFF) na Shirika la Development Aid From People to People (ADPP - Mozambique)

MATUKIO KATIKA PICHA

Kijana akichangia hoja wakati wa mdahalo

Mratibu wa Masuala ya Watoto AGPAHI mkoa wa Shinyanga ,Dk. Jane Kashumba akielezea lengo la Malumbano hayo ya hoja kwa vijana.

Kila mshiriki wa Malumbano ya Hoja alipewa zawadi ya begi la shule: Katikati ni Kaimu Mratibu wa Ukimwi mkoa wa Shinyanga Sherida Madanka akimkabidhi mabegi mmoja wa vijana walioshiriki malumbano ya hoja ili awagawie wenzake.

Vijana wakiwa ukumbini

Picha ya pamoja mgeni rasmi,wafanyakazi wa shirika la AGPAHI na vijana walioshiriki katika malumbano ya hoja.
 
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

 

More on News

Get Connected