MAHUSIANO YA KIMAPENZI BILA KUPIMA AFYA YADAIWA KUWA CHANZO KIKUBWA CHA MAAMBUKIZI YA VVU

Imeelezwa kuwa watu wengi wanaendelea kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutokana na kuanza mahusiano ya kimapenzi bila kutambua afya zao hali inayosababisha waanze kuishi kama mume na mke bila kujua hali zao za kiafya.

Hayo yamesemwa leo Februari 14,2018 na wahudumu wa jamii wanaosaidia kazi katika vituo vya tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na Maambukizi ya VVU vilivyopo katika halmashauri 7 za wilaya mkoani Mwanza yanayofanyika katika ukumbi wa hotel ya Midland jijini Mwanza.

Wahudumu hao wapo katika mafunzo ya msaada na huduma za kisaikolojia yanayotolewa na Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia Centres for Disease Control (CDC).

Wahudumu walisema kitendo cha kuanza mahusiano ya kimapenzi na kuoana bila kutambua afya ni miongoni mwa tabia hatarishi zinazochangia kwa kiasi kikubwa kuambukizana VVU. 

Mmoja wa washiriki hao Chausiku Sitta kutoka halmashauri ya wilaya ya Kwimba alieleza kuwa vijana wanapata maambukizi ya VVU kutokana na kukosa elimu sahihi juu ya VVU na Ukimwi na wengi wao kutawaliwa na tamaa ya ngono isiyo salama na kudhani kuwa kila mtu anayeonekana kuwa na umbo zuri basi hana maambukizi ya VVU.

“Vijana wanakurupuka tu,tena wakiona mwanaume ana mvuto ama mwanamke ana makalio makubwa wao wanaita ‘wowowo’ wanachanganyikiwa kabisa,ndugu zangu huwezi kumtambua mtu mwenye maambukizi ya VVU kwa kumwangalia kwa macho mpaka apimwe”,aliongeza Chausiku.

Naye Musa Ordas kutoka halmashauri ya wilaya ya Buchosa aliitaka jamii kutoendekeza waganga wa jadi kwani baadhi yao wanawadanganya watu wanaoishi na VVU kuwa wamerogwa kwa kuwalaghai kuwa wametupiwa majini mahaba. 

Kwa upande wake, Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Dk. Joseph Musagasa aliwataka wanaume kuacha tabia ya kutumia majibu ya wake zao wanapopima VVU kwani majibu yanatofautiana na hutokea wakati mwingine mmoja kati yao kuwa na maambukizi na mwingine kutokuwa nayo. 

Dk. Musagasa aliwashauri akina mama kupima afya zao kabla ya kubeba ujauzito,na kujifungulia katika vituo vya afya ili kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. 

“Siyo watoto wote wanaozaliwa na mama mwenye maambukizi ya VVU wana VVU,hivyo mama unapotaka kubeba mimba pima kwanza afya yako,ukibainika una maambukizi utashauriwa na wataalamu wa afya namna ya kufanya ili usimwambukize mtoto wako”,alieleza Dk. Musagasa.

ANGALIA PICHA WAKATI WA MAFUNZO KUHUSU MSAADA NA HUDUMA ZA KISAIKOLOJIA KWA WAHUDUMU WA JAMII SIKU YA TATU

Mwezeshaji katika mafunzo ya msaada na huduma za kisaikolojia, Dk. Joseph Musagasa akielezea umuhimu wa kupima afya kabla ya kuanzisha mahusiano ya kimapenzi au kuingia katika ndoa.

 

Dk. Musagasa akizungumza wakati wa mafunzo hayo. Aliwataka watu wanaoishi na maambukizi ya VVU kuzingatia matumizi sahihi ya dawa zinazofubaza makali ya VVU pamoja na kuzingatia lishe bora.

Chausiku Sita kutoka kituo cha afya na matunzo cha hospitali ya Ngudu halmashauri ya wilaya ya Kwimba akielezea namna vijana wanavyopata maambukizi ya VVU kutokana na kukosa elimu sahihi kuhusu VVU na Ukimwi. Alisisitiza umuhimu wa kuwa muwazi unapobainika kuwa una maambukizi ya VVU.

Musa Ordas kutoka kituo cha afya Nyehunge kilichopo katika halmashauri ya wilaya ya Buchosa akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo.

Mhudumu wa afya kituo cha afya Sengabuye iliyopo katika halmashauri ya manispaa ya Ilemela, Bahati Balekele Boyi.

Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona akielezea faida za kuzingatia lishe bora kwamba inasaidia kuwa na afya njema

Cecilia Yona akielezea kuhusu madhara ya kutozingatia lishe bora.

PICHA ZA MATUKIO KWENYE MAFUNZO SIKU YA PILI

Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Gaston Kakungu ambaye ni Afisa Muuguzi Mstaafu akitoa mada kuhusu umuhimu wa kuwa muwazi unapopata maambukizi ya VVU.

Kakungu akiendelea na mada ya uwazi.

Washiriki wa mafunzo hayo wakifanya kazi za makundi.

Mshiriki wa mafunzo hayo Shija Mashimba kutoka kituo cha tiba na matunzo cha hospitali ya Rufaa ya Bugando akiwasilisha kazi ya kundi lake kuhusu tabia hatarishi zinazochangia kuwepo kwa maambukizi ya VVU,mfano kudanganywa na waganga wa kienyeji kwa kupewa dawa za kuongeza nyota zao.

Mhudumu ngazi ya jamii, Winfrida Meshack kutoka hospitali ya Sekouture akiwasilisha kazi ya kundi lake kuhusu tabia hatarishi zinasobabisha maambukizi ya VVU kama vile ngoma za usiku ambazo zinawakutanisha wanaume na wanawake.

 

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

 

 

 

 

More on News

Get Connected