SHIRIKA LA AGPAHI LAANZA KAMBI YA WATOTO NA VIJANA YA WIKI MOJA MJINI MOSHI – MKOANI KILIMANJARO

 

 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dr. Asha Mahita akiwa katika picha ya Pamoja na Vijana na Watoto Nje ya Ukumbi wa hotel ya Uhuru iliyopo Mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro.

Toka mwaka 2011 Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) limekua msaada mkubwa kwa watoto wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) nchini Tanzania. Shirika hili la kitaifa lisilo la Kiserikali lilianzishwa na shirika la Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation  (EGPAF) huku lengo kuu likiwa kutokomeza maambukizo ya virusi vya Ukimwi kwa watoto nchini Tanzania. Mpaka sasa AGPAHI ina takribani miaka saba, shirika hili limekua msaada mkubwa kwa watoto hao wanaoishi na VVU kutimiza ndoto zao. 

Kila mwaka Shirika la AGPAHI huandaa kambi ya watoto kutoka katika mikoa sita inayofanya kazi nayo ambayo ni Mikoa ya Tanga, Simiyu, Geita, Mwanza, Mara na Shinyanga. Kambi hiyo hukusanya watoto kutoka katika vikundi vya watoto na vijana ambavyo huundwa katika Vituo vya Afya husika. Watoto hao huudhuria katika vikundi ili kujifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa tiba na elimu kuhusu matumizi sahihi ya Dawa za Kupungua makali ya VVU (ARV’s). Vikundi hivyo huwezeshwa kwa msaada wa shirika la AGPAHI kupitia msaada wa watu wa Marekani.  Kupitia vikundi, watoto na vijana hupata fursa ya kuhudhuria kambi ya wiki moja inayoandaliwa na shirika la AGPAHI. 

 

Leo(12.03.2018) Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dr. Asha Mahita amefungua kambi ya wiki moja ya watoto na vijana katika Ukumbi wa Hotel ya Uhuru  Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro. Dr. Mahita alitumia nafasi hiyo kuzungumza moja kwa moja na watoto takribani hamsini (50) kutoka Mikoa mitatu ya Tanga, Mwanza na Geita ambao wamehudhuria kambi hiyo. Watoto na vijana wenye umri wa miaka 10 – 17.

“Fursa hii kwangu ni fursa adimu sana kukutana na watoto wengi kama ninyi wenye tumaini kuu na ari ya kutimiza ndoto, nawahakikishia kuwa siku moja mtasimama na kuidhihirishia jamii kwa vitendo kuwa mnaweza, Cha muhimu ni kuzingatia matumizi sahihi ya dawa na kuendelea kuwepo kwenye huduma.” Alisema Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Pia aliweza kukaa na watoto na kuzungumza nao kuhusu afya zao na kuwapa nafasi ya kuuliza maswali  kuhusu ufahamu wa  VVU / UKIMWI kitaalamu. Moja ya maswali hayo ni:- Njia za Maambukizi ya VVU, Faida ya kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU.

Hata hivyo AGPAHI waliweza kueleza dhumuni kuu la kambi hiyo kuwa ni kuwakutanisha watoto na vijana ili kujifunza mambo mbalimbali kuhusu afya, Kutoa ushauri wa  Kisaikolojia kwa watoto wanaoishi na VVU, lakini pia kuwasaidia uangalizi wa afya zao na maendeleo ya afya zao. Ambapo katika kambi hii kuna mtaalamu wa saikolojia ambaye wakati wote wa kambi atatoa nafasi ya kuzungumza na kila mtoto kwa wakati wake ili kuweza kufahamu na kutatua yale ambayo yanawakabili kitaalamu. Lakini pia katika kambi hii kuna Madaktari Bingwa wa watoto  ambao wakati wote watakua wakiwahudumia watoto katika kipindi chote cha kambi.

Muelemishaji rika, Douglas kutoka jijini Mwanza akiwaelezea watoto na vijana wakati wa ufunguzi rasmi wa kambi

AGPAHI wanaamini watoto kujifunza katika michezo ni moja ya eneo sahihi hivyo basi  wamewashirikisha wawezeshaji wa michezo ambao wameandaa mpango maalumu wa mafunzo kupitia michezo kwa siku zote za kambi hiyo.

Watoto na vijana wakiwa wanafnya mazoezi na michezo yaliondaliwa na kikundi cha "Sports for Change'

PICHA NA KILIMANJARO OFFICIAL BLOG

 

 

 

 

More on News

Get Connected