MGANGA MKUU WA MKOA WA MARA AFUNGUA KAMBI YA WATOTO NA VIJANA YA AGPAHI MJINI MOSHI

Jumatatu ya Tarehe, 11 Juni 2018 Shirika lisilo la Kiserikali la Arial Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) limeanza kambi maalumu ya watoto na vijana kwa Mikoa mitatu ya Tanzania ambayo ni Mara, Shinyanga na Simiyu, ambayo ni  kati ya Mikoa sita inayofanya kazi na shirika la AGPAHI. Kambi hiyo inayofahamika kwa jina la ARIEL CAMP  ni kambi ya kumi toka kuanzishwa kwa kambi hizi zenye lengo la kuwakutanisha watoto na vijana kutoka katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kujifunza kwa njia ya  michezo na kufanya matembezi katika sehemu mbalimbali kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo.

Picha ya pamoja na Mgeni rasmi wakati wa kufungua mafunzo ya watoto na vijana yanayotarajiwa kufanyika kwa muda wa siku tano kwaajili ya kuwajengea watoto na vijana uwezo wa kujithamini na kujiamini.

Afisa miradi huduma unganishi kwa jamii kutoka mkoa wa Mwanza Bi, Cecilia Yona kwa niaba ya shirika aliweza kumkaribisha mgeni rasmi, watoto na vijana pamoja na wale wote walioambatana nao katika kuhakikisha wanafanikisha lengo la kambi hiyo. Pia alizungumza kuhusu umuhimu wa kuwaweka watoto na vijana pamoja katika kuwapatia mafunzo ya darasani, michezo na kusema hii inawajengea watoto uwezo binafsi wa kujiamini zaidi na pia kuweza kushirikiana na wenzao katika mambo mbalimbali. Pia aliwasisitiza watoto wawe wasikivu na watulivu ili waweze kujifunza na kufurahia kambi hii yenye lengo zuri kwa maisha yao ya sasa na ya baadae.

Afisa miradi huduma unganishi kwa jamii kutoka mkoa wa Mwanza,  Bi, Cecilia Yona akiongea katika hafla ya ufunguzi wa ARIEL CAMP.

“Ni jukumu letu kuwasaidia watoto na vijana hawa, sababu ni vijana wenye moyo wa kujifunza  na wana ndoto kubwa ambazo wakipata watu wa kuwapa muongozo sahihi wataweza kufika mbali sana” Alisema Bi, Cecilia Yona.

ARIEL CAMP Juni 2018 ilifunguliwa na mgeni rasmi ambaye ni Mganga mkuu wa Mkoa wa Mara Dr. Francis K. Mwanisi, alifungua kambi hiyo ya watoto na vijana katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Uhuru Lutherani Hostel uliyopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, ambapo Camp hiyo yenye watoto na vijana 50 waliopo chini ya uangalizi wa
walezi na wauguzi 10, daktari bingwa wa watoto 1, mtaalamu wa saikolojia 1, walimu wa michezo 4, muelimishaji rika na wafanyakazi wa Shirika la AGPAHI  ambao watakua pamoja katika kipindi chote cha kambi.
Mbali na mafunzo ya darasani, watoto na vijana hao watapata fursa ya kutembelea maeneo kama Holili na Marangu kujifunza mambo mbalimbali zikiemo, mila na desturi za wachaga wanaoishi katika maeneo hayo watakayoyatembelea.

Mganga mkuu wa mkoa wa Mara, Dr. Francis K. Mwanisi, akiongea wakati wa kufungua mafunzo ya watoto na vijana katika hafla fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa Uhuru Lutherani uliopo Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dr. Mwanisi, katika hotuba yake aliweza kutoa pongezi kwa shirika la AGPAHI kwa kuchagua kundi hili la watoto na vijana kuweza kuwaweka pamoja, kuwapa elimu ya kujitambua, kujiamini, kujithamini na kujifunza kwa vitendo. Pia aliweza kuwashauri watoto na vijana kuzingatia yale wanayofundishwa katika kambi na waende wakawe mabalozi wazuri kwa watoto na vijana wenzao watakaporudi nyumbani.

Douglas almaarufu kama Uncle D, akiongea na watoto pamoja na vijana akiwashauri namna ambavyo wanatakiwa kuishi ili waweze kutimiza ndoto zao. 

Kisha Douglas almaarufu kama Uncle D, akapewa nafasi ya kuwashauri watoto na vijana namna ambavyo wanatakiwa kuishi ili waweze kutimiza ndoto zao. Ambapo alielezea namna ambavyo kambi zinaweza kuwasaidia watoto na vijana katika kufikia malengo yao endapo watazingatia yale wanayofundishwa. Pia aliwaelezea watoto na vijana wasikate tamaa endapo watakutana na changamoto zozote katika maisha yao.

“Naona mna ndoto kubwa sana na ndoto hizi mtaweza kuzifanikisha endapo mtasikiliza na kufuata yale mnayofundishwa katika kambi hii. Nawashauri watoto na vijana mjikubali, mjithamini na kujiamini bila kujali changamoto wanazopita katika maisha yenu ya kila siku” Alisema Uncle D.


PICHA ZOTE NA JOSHUA KILIBLOG

More on News

Get Connected