P.O Box
38252
Location
Tanzania
information@agpahi.or.tz
Telephone
+255 22 2600606
Sababu mojawapo kubwa ya kushuka kwa kinga ya mwili haswa katika nchi zilizopo chini ya jangwa la Sahara ni Ukimwi/VVU.Hata hivyo ieleweke kwmba si kila mtu mwenye upungufu wa kinga mwilini ana VVU.
Magonjwa nyemelezi si neno geni miongoni mwa watu wengi haswa katika miongo hii miwili toka kugundulika kwa ugonjwa wa Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) na Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Magonjwa nyemelezi ni yale ambayo hushambulia mwili wa binadamu pale uwezo wa kinga ya mwili kupigana na vimelea vya magonjwa unaposhuka.Ni magonjwa ambayo katika hali ya kawaida hayategemewi kujitokeza kwa mtu mwenye kinga kamili ya mwili.
Kwa kawaida mwili wa binadamu yeyote umeumbwa na kinga ya mwili ya asili ambayo lengo lake kuu ni kuulinda mwili dhidi ya vimelea vya magonjwa.Inapotokea kimelea (vimelea) kuingia katika mwili wa binadamu kwa njia yoyote (kunywa au kula vimelea,kugusana na majimaji au ngozi ya mtu mwenye vimelea,au kupitia damu yenye vimelea n.k), mwili hutengeneza kingamwili (antibodies) ambazo hupigana na vimelea hivyo ili kuuweka mwili katika afya njema kama hapo awali.
Kushuka kwa kinga ya mwili hupelekea mwili kushindwa kupigana na vimelea vya magonjwa hivyo kusababisha kushambuliwa na magonjwa.Ifahamike kwamba baadhi ya vijidudu(microorganisms) pia hupatikana katika mwili wa binadamu bila madhara yoyote (normal flora) kama vile kwenye ngozi, mfumo wa chakula, ukeni, uumeni n.k Hata hivyo vijidudu hivi huweza kuwa chanzo cha magonjwa iwapo kinga ya mwili itashuka.
Magonjwa nyemelezi husababishwa na vijidudu mbalimbali kama bacteria,virusi,fangasi na bakteria.
Kandidiasisi
Ugonjwa huu uliozoeleka pia hujulikana kwa kitaalamu kama Candidiasis.Kandidiasisi husababishwa na fangasi aitwaye Candida albicans ambaye huathiri kinywa, mfumo wa chakula,uke na mfumo wa hewa.Kandidiasisi katika uke huweza tokea kwa mwanamke mwenye afya asiye na VVU.
Dalili za Kandidiasisi katika kinywa ni pamoja na kubadilika kwa ladha,maumivu kwenye ulimi,utando mweupe kwenye ulimi na kingo za juu za kinywa (buccal mucosa),kushindwa kumeza,maumivu wakati wa kumeza chakula ikiwa fangasi imesambaa sana. Pia mwasho na maumivu ukeni pamoja na kutokwa na majimaji meupe ukeni.
Homa ya Uti wa mgongo
Homa ya uti wa mgongo au Meningitis kwa kitaalamu husababishwa na fangasi aitwaye Cryptococcal neoformans.Uti wa mgongo utokanao na aina hii ya fangasi huweza kusababisha kifo usipotibiwa.Aina hii ya fangasi ambayo huathiri zaidi ubongo na uti wa mgongo, hutokana na kuvuta hewa yenye vumbi litokanalo na ndege lenye vimelea vya ugonjwa.
Baadhi ya dalili zake ni homa, kutoona vizuri,macho kuuma kutokana na mwanga,kuchanganyikiwa akili,maumivu ya kichwa ka kukakamaa na kuuma kwa shingo.
Histoplasmosisi
Aina hi ya fangasi hutokana na vimelea vya Histoplasma capsulatum.Fangasi huyu huathiri mapafu pamoja na viungo vingine.Dalili zake ni homa,uchovu,kupungua uzito na kupumua kwa shida.Pia kukohoa na kuvimba kwa tezi kwaweza kutokea.
Nimonia
Kama bakteria na fangasi pia huweza kusababisha nimonia ijulikanayo kwa kitaalamu kama Pneoumocystis Pneumonia (PCP).Vimelea vya Pneumocystis jiroveci (awali vilijulikana kama Pneuomocystis carinii) huathiri mfumo wa hewa.Fangasi huyu pia huweza kuathiri viungo vingine kama ini,wengu (spleen) na figo katika baadhi ya wagonjwa.
Dalili zake ni kikohozi kikavu,kifua kubana,kupumua kwa shida,homa,kuishiwa pumzi na kutokwa jasho nyakati za usiku.
Toksoplasmosisi ya Ubongo
Cerebral toxoplasmosis, kama ujulikanavyo kitaalamu,hutokana na kuamshwa kwa ugonjwa wa awali kutokana na vimelea vya Toxoplasma gondii (kimelea kiwezacho kuishi ndani ya seli kinachoathiri ndege,wanyama na binadamu).Kimelea hiki kiathiricho zaidi mfumo wa fahamu,hupatikana kwenye nyama isiyopikwa vizuri na mavi ya paka.Huathiri zaidi ubongo na kusababisha maumivu ya kichwa,kuchanganyikiwa,udhaifu wa viungo,homa,kupoteza fahamu,kupooza na kifafa.
Kriptosporidiosisi
Huu ni ugonjwa utokanao na vimelea vya Cryptosporidium.Huathiri zaidi mfumo wa chakula na hutokana na kutumia kwa maji au chakula vilivyoathirika na vimelea vya ugonjwa huu.Dalili zake ni kuharisha sana kiasi cha kusababisha kupungukiwa na maji mwilini (dehydration),maumivu wakati wa haja kubwa, kichefuchefu na kutapika.Wagonjwa wa aina hii huwa na joto la mwili la kawaida.
Matibabu na Ushauri
Aina ya matibabu hutegemea na aina ya ugonjwa na mtu, pia kutokana na kuwepo kwa Ukimwi/VVU hutegemea kiwango cha seli za CD4 mwilini.Iwapo una dalili kati ya zilizotajwa hapo juu ni vyema kumona daktari kwa uchunguzi zaidi.
Ni vyema kuzingatia kuwepo kwa dalili zilizotajwa hapo juu hakumanishi kuwa muathirika ana VVU na si kila mwenye VVU huwa na dalili hizo.Pia kujitokeza kwa dalili kunaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu.Hata hivyo ni vyema kupima afya yako kila mara haswa VVU ili kujua chanzo cha kupungua kwa Kinga ya mwili ambayo huweza kupelekea kupata magonjwa nyemelezi
Ni vizuri kwenda kupima katika hospitali na vituo vya huduma ili kugundua hali yako ya afya na kufuata ushauri nasaha.
Inachukua siku 90(miezi mitatu) kwa VVU kuonekana, ndio maana ni vizuri kurudi kupima siku ya 90 baada ya kupata vipimo vya kwanza vya VVU.